Na Mwandishi Wetu,
DODOMA.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel leo Jumamosi Aprili 05, 2025 Akiwa Mjini Dodoma wakati wa Uzinduzi wa Jengo la makao makuu ya Mahakama ya Tanzania, linalozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, amesema Jengo hilo linaweka rekodi ya kuwa Jengo kubwa zaidi barani Afrika na la sita kwa ukubwa duniani.
"Jengo hili lipo kwenye kiwanja ambacho kina ukubwa wa hekta 18.9 sawa na hekari 45.5. Mhe. Rais jengo hili limejengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 129.7 na lina ukubwa wa ghorofa tisa na jumla ya sakafu zake ukizijumlisha inakuwa na ukubwa wa mita za mraba za square Mita 63, 244."
Wakati wa uzinduzi wa Jengo hilo leo Aprili 05, 2025 Jijini Dodoma mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, mtendaji huyo amesema "Pamoja na Mambo mengine Mhe. Rais jengo hili lina vifaa vya kisasa vya tehama pamoja na eneo maalum kwaajili ya kutua Helkopta.
"Mhe. Rais kwa maana ya jumla ya sakafu yaani zile mita za mraba 63,244 ni sawa na shamba la kawaida la hekari 13 kwahiyo hili ni jengo kubwa sana na kwa ulinganifu na majengo mengine duniani, jengo la kwanza kwa ukubwa wa mita za mraba kwenye sakafu lipo barani Asia likiwa na ukubwa wa sakafu square Mita 147,000, la pili mpaka la sita yapo ulaya ambapo la sita lina ukubwa wa sakafu 53,000 na letu hili unalotuzindulia hapa Mhe. Rais lina ukubwa wa sakafu square mita 63, 244. Maana yake Mhe. Rais leo jengo hili unalotuzindulia leo hapa linakuwa la sita kwa ukubwa wa sakafu na la kwanza barani Afrika" - amesema Ole Gabriel.
Aidha akizungumzia miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali ya awamu ya sita kwa miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, Mtendaji huyo wa mahakama ameeleza kuwa kwa miaka minje jumla ya Bilioni 146. 16 zimetolewa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo imekamilika na mingine ikiendelea kutekelezwa, huku miradi ya leo ambayo ni Jengo la tume ya utumishi wa mahakama, makazi ya Majaji na Jengo hilo la makao makuu ya mahakama vikigharimu takribani Shilingi Bilioni 185 za Kitanzania.
0 Comments