HEADLINES

6/recent/ticker-posts

AFRICA THINK TANK NA ARTHSHAKTI WASHIRIKIANA KUINUA MAENDELEO YA JAMII NA KILIMO


 Na AMEDEUS SOMI,
DAR ES SALAAM.

Taasisi ya Afrika Think Tank (ATTF) imeingia ubia na Taasisi ya Arthshakti kwa lengo la kushirikiana katika kuinua maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini, hususan kwenye sekta za kilimo, afya, elimu ya fedha na maendeleo ya kidijitali.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kusaini mkataba wa makubaliano baina ya taasisi hizo, Mwanzilishi na Mwenyekiti Mtendaji wa ATTF, Bi. Elizabeth Riziki, alisema ushirikiano huo utasaidia juhudi za Serikali katika kukuza maendeleo jumuishi na kuimarisha maisha ya wananchi.

“Tutajikita kwenye maeneo ya kilimo kwa kutoa elimu ya biashara na masoko kwa wakulima, mazingira, afya na matumizi sahihi ya intaneti. Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wananufaika na teknolojia za kidijitali katika kuboresha maisha yao ya kila siku,” alisema Riziki.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Arthshakti, Bw. Somesh Kulshrestha, alisema wataunga mkono jitihada za ATTF kupitia miradi ya afya, elimu na kilimo.

“Tutashirikiana katika miradi ya afya itakayopunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa. Pia tutatoa na kufundisha matumizi ya kompyuta kwa wanafunzi katika shule mbalimbali nchini, sambamba na elimu ya kilimo,” alisema Kulshrestha.


Naye Katibu Mtendaji wa Arthshakti, Bi. Mira Solanki, alibainisha kuwa taasisi hiyo itaandaa kambi maalum za kilimo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wakulima juu ya matumizi ya pembejeo, viuatilifu, afya za wakulima pamoja na mbinu za kuongeza tija.

“Mkulima ana haki ya kuishi maisha bora kama watu wengine. Kupitia ubia huu, tutawasaidia wakulima kupata mikopo, huduma za afya na mbinu rahisi za kilimo zitakazowawezesha kuzalisha kwa ufanisi zaidi,” alisema Solanki.


Ushirikiano huo unatarajiwa kuchochea mageuzi katika sekta za kilimo, elimu na afya, huku ukilenga pia kuimarisha matumizi sahihi ya teknolojia ya kidijitali kwa maendeleo ya taifa.

 

Post a Comment

0 Comments