Na Mwandishi Wetu,
PWANI.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Uchukuzi na Shirika la reli Tanzania TRC kuboresha Vitengo vyao vya Mauzo na biashara, kwa kuweka watu wenye weledi na wabunifu katika kuhakikisha tija inapatikana katika usafirishaji wa Mizigo kupitia reli ya kisasa ya SGR.
Rais Samia amebainisha hayo leo Alhamisi Julai 31, 2025 wakati wa uzinduzi wa Usafirishaji wa mizigo kwa reli ya SGR, Kuweka jiwe la msingi kwenye Kongani ya Viwanda Kwala pamoja na uzinduzi wa Kituo cha Kimataifa cha Lojistiki Kwala, akieleza kuwa kuzinduliwa kwa Vitu hivyo ni mwanzo wa Kuifanya Tanzania kuwa Kitovu cha Usafirishaji Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
"Matukio haya yote matatu ya Kimkakati ni mwanzo wa safari yetu ya kuifanya Tz kuwa kitovu cha usafirishaji wa biashara kanda ya Afrika Mashariki na kati. Maendeleo haya makubwa yanaashiria sura mpya ya nchi yetu, Tanzania ya viwanda yenye miundombinu ya kisasa na yenye kujikita katika uchumi shindani wa Kikanda na Kimataifa." Amesema Rais Samia.
Katika maelezo yake, Rais Samia pia ameiagiza Wizara ya Uchukuzi kushirikiana na Wazalishaji wakubwa wa ndani na nje ya nchi ili kuwavutia kutumia usafiri wa SGR kusafirisha mizigo yao, akionesha kufurahishwa na Wafanyabiashara wakubwa na Makampuni ya GSM na Bakhresa kuanza kutumia usafiri huo wa SGR.
Rais Samia ameeleza kuwa kuzinduliwa kwa safari hizo za Mizigo ni ushahidi wa namna Tanzania ilivyoamua kwa dhati kuimarisha mifumo ya usafirishaji wa mizigo nchini kuanzia kwenye usafiri wa barabara, Usafiri wa anga, Usafiri wa Majinu na usafiri wa reli.
Ameeleza kuwa kuanza kusafirisha mizigo kwa reli ya SGR kutoka Dar Es Salaam kwenda Dodoma ni mkakati wa Kitaifa wa kupunguza gharama za usafirishaji, kuepusha uchakavu wa barabara na kulinda mazingira, akisema usafiri huo pia umepunguza muda wa usafirishaji wa mizigo kutoka saa 30/35 kwa Magari ya Mizigo kutoka Dar Es Salaam hadi Dodoma hadi kufikia saa 4/5 kwa reli ya Kisasa SGR.
Aidha Usafirishaji huo pia kulingana na Rais Samia utapunguza msongamano wa magari Jijini Dar Es Salaam pamoha na kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar Es Salaam kwa kupunguza muda wa kushusha na kupakia mizigo katika bandari hiyo tegemeo kwa nchi zinazoizunguka Tanzania.
0 Comments