HEADLINES

6/recent/ticker-posts

TABWA YAJA NA CLEAN COOKING MARATHON 2025 KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA


 Na Mwandishi Wetu,
DAR ES SALAAM.

Jumuiya ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TABWA) imetangaza rasmi kuandaa mbio maalum za Clean Cooking Marathon 2025 kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa kuelekea lengo la Taifa la asilimia 80 ya matumizi ya nishati hiyo ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mbio hizo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alisema mbio hizo ni za kihistoria na zinaendana na juhudi za serikali katika kuimarisha afya ya jamii na kutunza mazingira kupitia matumizi ya nishati safi.
“Mimi nitashiriki mbio hizi. Naamini Clean Cooking Marathon haitakuwa ya mwisho kwa kuwa kwa muda mrefu hatujawahi kuwa na mbio zenye ajenda ya nishati katika Mkoa wa Dar es Salaam,” alisema Mtambule.

Aliongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, huku mwaka jana Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, akizindua Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia.
“Marathon hii inatoa nafasi ya kipekee kuhamasisha ajenda hii muhimu inayogusa afya, maendeleo, na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,” alisema.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), William Kalaghe, alisema RT inaunga mkono kampeni hiyo na kwamba mchezo wa riadha ni jukwaa lenye nguvu kufikisha ujumbe wa kijamii.
 
“Tunawashukuru TABWA kwa kutuchagua kama wadau wa kushirikiana nao. Wangeweza kuchagua njia yoyote, lakini wameona riadha inaweza kufanikisha kufikisha ujumbe huu kwa jamii,” alisema Kalaghe.
Naye Mkurugenzi wa TABWA, Noreen Mawalla, alisema kuwa mbio hizo ni sehemu ya azimio la kongamano la kwanza kuhusu nishati safi lililofanyika Juni 2023, ambapo TABWA ilishirikiana na kampuni ya Oryx kutoa elimu na kugawa majiko ya gesi kwa mama lishe 250 kutoka Dar es Salaam na Pwani.
“Tumeamua kushiriki kikamilifu katika ajenda ya nishati safi kwa sababu wanawake na watoto ndio waathirika wakuu wa nishati isiyo salama. Clean Cooking Marathon ni kampeni endelevu itakayofanyika katika kanda sita nchini kuanzia Aprili 26, 2025, ikihusisha pia utoaji wa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na uchangishaji wa fedha kwa ajili ya kuendeleza kampeni hii,” alisema Noreen.

 Aidha, alisema mgeni rasmi katika mbio hizo anatarajiwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, huku jezi rasmi za marathon hiyo zikipatikana kwa gharama ya Shilingi 35,000.

TABWA ni taasisi iliyoanzishwa kisheria Februari 1, 2019, ikilenga kusaidia wanawake na vijana kupitia mafunzo ya ujasiriamali, program za ushauri na kukuza biashara. Kupitia Clean Cooking Marathon, taasisi hiyo inalenga kuunga mkono jitihada za serikali katika kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi, kwa manufaa ya afya, mazingira na ustawi wa Taifa kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments