Na Mwandishi Wetu,
TANGA.
Wadau mbalimbali wamemchangia Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Ummy Mwalimu, fedha kiasi cha Shilingi 1,300,000, ili zimuwezeshe kuchukua fomu ya Ubunge ili agombee tena nafasi hiyo kwa kipindi kingine katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu
Fedha hizo ni matokeo ya michango ya hiari kutoka kwa wadau kama vile Taasisi ya Mguu Kwa Mguu, Friends of Odo Ummy, Sema na Tanga na watu wengine nje na taasisi hizo.
"Mheshimiwa Mbunge wetu Ummy Mwalimu, napenda kukukabidhi Shilingi 1,300,000 kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo Tanga ambao wamejichangisha wao wenyewe ili zisaidie kulipia fomu ya Ubunge. Kwa kweli tunaridhishwa na utendajikazi wako na namna unavyotatua kero za wananchi. Katika kipindi cha uongozi wako, Jimbo la Tanga Mjini limepata miradi mingi ya maendeleo, kwa kweli umefanya makubwa, tunatamani urudi tena madarakani uendelee kuwatumikia wananchi wako," amesema Mukulu.
Vilevile, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sema na Tanga, Said Massa, amesema Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 Tanga Mjini imetekelezwa ipasavyo, hivyo anaunga mkono zoezi la kumchangia fomu ya Ubunge Ummy Mwalimu ili aendeleze kazi nzuri.
"Kwa kweli Jimbo la Tanga Mjini limenufaika sana na uongozi wako ulioacha alama katika maisha ya wananchi kwani umetekeleza miradi mingi ya maendeleo kama vile maji, afya, elimu, Bandari ya Tanga, umeme, barabara na miradi mingine mingi," amesema Massa.
Elias Mpayi ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Mguu Kwa Mguu amesema Ummy Mwalimu amewezesha Tanga Mjini kupata maendeleo makubwa katika kipindi kifupi cha uongozi wake, hivyo anastahili kuongoza kwa mara nyingine.
Baada ya makabidhiano hayo, Ummy Mwalimu, amewashukuru wadau hao waliojitoa kwa hali na mali kumchangia fomu ya Ubunge kwani bado ana dhamira ya kuendelea kuwatumikia wananchi wa Tanga Mjini.
0 Comments