Na Amedeus Somi,
Maelezo.
Mkurugenzi wa bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari Wakili Msomi Patrick Kipangula, amesema ni kosa la jinai kwa waandishi wa habari kufanya kazi hiyo bila kuwa na ithibati.
Kipangula amesema hayo wakati akiwasilisha mada katika mkutano wa wadau wa sekta ya habari na utangazaji kanda ta mashariki, kuelekea uchaguzi mkuu 2025.
"Ukisoma kifungu cha 19 cha sheria ya huduma za habari inaeleza kuwa mtu yoyote anayetaka kufanya kazi za uandishi wa habari ni lazima awe amepewa ithibati na bodi ya ithibati ya waandishi wa habari, kwa hiyo hakuna mtu yoyote anaruhusiwa kufanya kazi yoyote ya kihabari isipokuwa tu awe amepewa ithibati na bodi ya ithibati wa waandishi wa habari, kwa hiyo katika kuelekea uchaguzi mkuu, waandishi ambao wanataka kufanya kazi ya kuripoti taarifa za uchaguzi wahakikishe wamepewa ithibati" amesema Bw. Kipangula.
Amesema kifungu cha (50) cha sheria kufanya kazi ya uandishi wa habari bila ithibati ni kosa la jinai, kwa hiyo kama ni kosa la jinai maana yake watu ambao wanakiuka hiyo sheria wanaweza wakapambana na Makamanda wa Polisi.
"Kwamba unafanya kazi kinyume na sheria ni kosa la jinai na ukipelekwa mahakamani ukikutwa na hatua adhabu yake ni kifungo cha miaka mitatu au kulipa faini ya shilingi millioni 5 hivyo ni muhimu kupata ithibati ili uweze kufanya kazi ya uandishi wa habari" amesema Bw. Kipangula.
Aidha Wakili Kipangula ametaja vigezo kwa wanaotakiwa kupewa ithibati, ni elimu ya kuanzia ngazi ya stashahada ya uandishi wa habari au elimu inayofanana na hiyo ambapo pia ametaja makundi yanayotakiwa kupewa ithibati ikiwemo waandishi wa habari, wahariri, watangazaji wa vipindi vya redio na runinga, wapiga picha na wale waandishi wa kujitolea.
Aidha Wakili kipangula ametaja haki za waandishi wa habari wakati wa uchaguzi ambapo amesema, kwa mujibu wa kifungu cha 7 (1) a cha sheria ya huduma za habari sura ya 229 (rejeo la 2023), mwandishi wa habari ana haki ya msingi ya kutafuta, kupokea na kutangaza habari bila ya kizuizi kwa kadiri ambavyo utekelezaji wa haki hiyo haukiuki madharti ya sheria, maadili ya taaluma ya uandishi wa habari na misingi ya maslahi ya umma.
0 Comments