HEADLINES

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YABORESHA SHERIA ZA HABARI, YAHAKIKISHA USHIRIKI WA VYOMBO UCHAGUZI MKUU


 

Na Amedeus Somi,

Maelezo,

Serikali imeahidi kuendelea kulinda uhuru wa vyombo vya habari na kuhakikisha tasnia hiyo inashiriki kikamilifu kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, katika mkutano wa wadau wa sekta ya habari na utangazaji kanda ya mashariki kuelekea uchaguzi mkuu 2025.

Akzungumza Jijini Dar es Salaam kwakati akifungua  mkutano wa Wadau wa Habarina Utangazaji kanda ya Mashariki Kuelekea Uchaguzi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Prof. Palamagamba Kabudi amesema jitihada za marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari Sura ya 229 zimeongeza uwazi, ufanisi na kuimarisha imani ya umma kwa tasnia ya habari ambapo marekebisho hayo yalifanywa kwa kushirikiana na wadau na yamechangia ongezeko la vyombo vya habari ikiwemo redio, televisheni, magazeti, blogu na mitandao ya habari mtandaoni.

Aidha Waziri Kabudi ameeleza kuwa zaidi ya waandishi wa habari 3,500 tayari wamesajiliwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari na wameanza kupata vitambulisho vya kazi (Press Cards). ametoa wito kwa waandishi wengine kuhakikisha wanajisajili ili kutambuliwa rasmi na kutekeleza majukumu yao kwa uhuru na weledi.

Amesema kwa  upande wa uchaguzi Serikali imetunga Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani zote za mwaka 2024, ambazo zimeondoa nafasi ya Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia uchaguzi na kuweka utaratibu wa kupata wasimamizi wenye sifa maalum. Sheria hizo pia zimeondoa utaratibu wa mgombea kupita bila kupingwa na kutoa haki mpya kwa makundi maalum kushiriki uchaguzi, wakiwemo wafungwa, mahabusu na wanafunzi wa vyuo vya mafunzo.

Waziri amewakumbusha waandishi wa habari umuhimu wa kuzingatia maadili ya taaluma yao ikiwemo kuepuka habari za upendeleo, uzushi, uchochezi na kuepuka vitendo vya rushwa maarufu kama ‘bahasha ya kahawia’. amesisitiza kuwa rushwa katika tasnia ya habari huondoa uaminifu, hudhoofisha demokrasia na kuhatarisha maisha ya waandishi waadilifu.

“Katika kipindi hiki cha uchaguzi, waandishi wa habari mnahitaji kuwa wazalendo wa kweli, wajenzi wa maelewano na wasimamizi wa uwajibikaji wa kisiasa,” amesema.

Aidha, alitoa wito kwa Jeshi la Polisi kushirikiana na vyombo vya habari kulinda usalama wa waandishi wakati wa kampeni na upigaji kura, huku akiwataka wanahabari nao kuheshimu sheria na kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

Kwa upande mwingine waziri amewasihi viongozi wa vyama vya siasa kutumia vyombo vya habari ipasavyo kufikisha sera na mipango yao kwa wananchi bila kuathiri mshikamano na amani ya taifa.

Akihitimisha, alisisitiza umuhimu wa kulinda amani ya nchi na kuwatanguliza maslahi ya taifa badala ya binafsi.

Post a Comment

0 Comments