Na Mwandishi Wetu
BAADA ya zoezi la kupiga kura kufanyika Oktoba 29, 2025, Watanzania walikuwa na matarajio makubwa ya kushuhudia mwendelezo wa demokrasia iliyokomaa.
Wananchi walijitokeza katika vituo vya kupigia kura kuchagua Rais, wabunge, madiwani na wawakilishi kwa upande wa Tanzania Zanzibar kwa utulivu na nidhamu.
Hata hivyo, katika baadhi ya maeneo hasa majiji na miji mikubwa, hali hiyo iligeuka ghafla baada ya watu wachache kuanzisha vurugu, kuvamia na kuharibu vituo vya kupigia kura, maduka, vituo vya mafuta na hata kufanya uporaji mitaani.
Kitendo hicho, ambacho kiliwacha taifa likiwa katika hali ya taharuki, kilisababisha vifo, majeruhi na uharibifu mkubwa wa mali. Wakati vurugu hizo zikiendelea, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camilius Wambura alitangaza amri ya kutokuwa barabarani kuanzia saa 12:00 jioni, isipokuwa kwa askari na wale waliokuwa wanatekeleza majukumu ya kiusalama.
Hatua hiyo ilikuwa muhimu, lakini pia ilionesha ukubwa wa tishio lililosababishwa na wachache waliodhamiria kuvuruga amani ya wengi.
Tangazo hilo la tahadhari liliendelea hadi leo, Novemba 3, 2025, pale ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alipoamuru kurejea kwa shughuli zote katika hali ya kawaida muda mfupi baada ya kuapishwa rasmi kuongoza Tanzania kwa kipindi kingine cha miaka mitano huko Chamwino, mkoani Dodoma.
Athari za vurugu hizo zimegusa kila sekta ya maisha ya Watanzania. Wakati wa amri ya kutokuwa barabarani, shughuli za biashara zilisimama kabisa.
Maduka na masoko yalifungwa, wafanyabiashara walipoteza mapato na bidhaa muhimu hazikufika kwa walaji. Vituo vya mafuta vilivyovunjwa vilisababisha uhaba mkubwa wa nishati, huku usafiri wa majini jijini Dar es Salaam ukisitishwa kwa muda. Watu waliokuwa wakihitaji matibabu hospitalini au huduma za dharura walikwama, wakikosa usafiri.
Hali hiyo ilileta maumivu makubwa kwa familia nyingi. Wazazi walishindwa kuwapeleka watoto hospitalini, wagonjwa waliokuwa wakihitaji uangalizi maalum walipata tabu na hata maiti katika hospitalini hazikuweza kupelekwa makaburini kwa wakati. Kwa maneno mengine, vurugu hizo zilisitisha mzunguko wa maisha ya taifa lote.
HATUA SERIKALINI
Baada ya tangazo la IGP Wambura, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka alitoa taarifa kwa umma akiwataka watumishi wa serikali kufanya kazi wakiwa majumbani kwao, huku wanafunzi wakitakiwa kujisomea nyumbani badala ya kwenda shuleni au vyuoni.
Hatua hii ya tahadhari ililenga kulinda usalama wa wananchi, lakini pia iliashiria uzito wa athari za vurugu zilizokuwa zimejitokeza.
Ni wazi kuwa nchi ilisimama. Miji mikubwa kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya iligeuka tulivu kwa hofu. Magari machache yaliyokuwa barabarani yalikuwa ya vyombo vya ulinzi na wananchi walibaki majumbani mwao wakisubiri maelekezo mapya kutoka mamlaka husika.
HASARA KIUCHUMI
Katika baadhi ya maeneo, vituo vya mafuta viliteketezwa kwa kuchomwa moto, vituo vya polisi na magari ya umma yalichomwa moto na maduka ya wafanyabiashara wadogo na wa kati yalivunjwa.
Takwimu za awali zinaonesha kuwa mamilioni ya shilingi yamepotea, huku mamia ya watu wakibaki bila ajira.
Virugu hizi zimeathiri pia mtiririko wa mapato ya serikali. Kodi ambazo zilikuwa zikikusanywa kutokana na biashara na usafirishaji sasa zimepungua. Wakati huo huo, serikali inalazimika kutumia fedha nyingi kurekebisha miundombinu iliyoathirika, fedha ambazo zingeweza kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo, elimu au afya.
VIFO NA MAJERUHI
Taarifa za awali zilizodokezwa na Rais Samia Suluhu Hassan muda mfupi baada ya kula kiapo cha kuiongoza tena nchi kwa kipindi kingine cha miaka mitano, zinaeleza kuwa watu kadhaa wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa katika machafuko hayo. Mkuu wa Nchi hajataja idadi yao.
Kila kifo ni pigo kwa taifa, kwa sababu nyuma ya kila aliyeuawa kuna familia, marafiki na jamii inayomlilia. Ni huzuni kubwa kwamba hasira za wachache zimegeuka kuwa kilio kwa wengi.
Vurugu hazina mshindi. Wale wanaoanzisha fujo mara nyingi hujificha au hukimbia, lakini waathirika hubaki wakibeba maumivu ya maisha yao yote. Ndiyo maana, kila Mtanzania anapaswa kufahamu kuwa kudumisha amani ni jukumu la pamoja na ukimya wetu mbele ya vurugu ni kibali kwa waharibifu kuendelea.
UMUHIMU WA USHIRIKIANO
Katika kipindi cha taharuki, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, limeonesha uthabiti mkubwa kuhakikisha hali inarejea katika utulivu.
Hata hivyo, mafanikio haya hayawezi kudumu bila ushirikiano wa wananchi. Tunapaswa kutoa taarifa mapema kuhusu viashiria vya uvunjifu wa amani, kukataa kushiriki katika maandamano haramu au matamko ya uchochezi na kusimama kidete kulinda maslahi ya taifa.
Ni wakati wa kutambua kuwa amani si jukumu la serikali peke yake, bali ni wajibu wa kila raia. Kila mmoja wetu ni askari wa amani - katika familia, mtaa na pahali pa kazi.
SOMO KWA TAIFA
Matukio ya Oktoba 29 na siku zilizofuata ni funzo kali kwa taifa. Amani tunayojivunia leo ni zao la nidhamu na busara za viongozi wetu tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere. Tukiruhusu wachache kuharibu utulivu huu, tutakuwa tunavunja msingi uliotupeleka mbele kama taifa.
Serikali, vyama vya siasa na taasisi za kiraia lazima zichukue hatua ya pamoja kufanya tathmini ya nini kilisababisha vurugu hizo, ili kurekebisha mianya ya chuki, upotoshaji na ukosefu wa maadili ya kisiasa.
Leo, Novemba 3, 2025, tunaposhuhudia Rais Samia akirejesha nchi katika hali ya kawaida, ni fursa ya kujitafakari kama taifa. Tujifunze kwamba amani ni gharama, na vurugu ni hasara isiyolipika.
Ni jukumu la kila Mtanzania kulinda utulivu huu uliopatikana kwa juhudi kubwa. Tusiache hasira za wachache zitawale akili za wengi. Badala yake, tuimarishe umoja, tukubali tofauti zetu za kisiasa kwa heshima na tuweke mbele maslahi ya taifa.
Tanzania ni yetu sote - tuilinde, tuiheshimu na tuipe thamani inayostahili.


0 Comments