
Na Mwandishi Wetu
WATANZANIA wamepita katika siku chache za majaribu makubwa baada ya vurugu zilizozuka wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, uchaguzi uliolenga kumchagua Rais, wabunge, madiwani na wawakilishi kwa upande wa Tanzania Zanzibar.
Badala ya kuendelea kuwa mfano wa demokrasia ya amani kama ilivyo desturi ya taifa letu, baadhi ya miji mikubwa ilijikuta ikizingirwa na fujo, uharibifu wa mali, majeruhi na hata vifo.
Vurugu hizo ziliwaacha wananchi wakiwa na hofu, biashara zikidorora na maisha ya kila siku yakisimama.
Hatua iliyochukuliwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camilius Wambura, ya kuwazuia wananchi kutokuwa barabarani kuanzia saa 12:00 jioni, ilisaidia kuzuia madhara zaidi, lakini pia iliashiria ukubwa wa tatizo lililosababishwa na wachache wasio na hekima.
Hata hivyo, leo, Novemba 3, 2025, hali imeanza kurejea katika utulivu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza rasmi kurejesha shughuli zote katika hali ya kawaida, muda mfupi baada ya kula kiapo cha kuongoza nchi kwa miaka mitano mingine huko Chamwino, Dodoma.
VURUGU NI ADUI WA USTAWI
Vurugu, kwa kiwango chochote, ni adui wa maendeleo. Zinafifisha ustawi wa taifa na kuhatarisha maisha ya watu wasio na hatia. Hali iliyojitokeza katika siku chache zilizopita ni somo tosha kwamba amani si jambo la kubahatisha.
Takwimu za awali zinaonesha kuwa mali nyingi zimeharibiwa, watu wamejeruhiwa na wengine wamepoteza maisha. Wengine wamepoteza ajira kutokana na biashara zao kuharibiwa, huku familia zikikosa kipato. Wakati wahalifu wachache wakitenda fujo kwa visingizio vya kisiasa, maumivu yake yamebebwa na wananchi wengi wasiokuwa na hatia.
Katika kipindi cha tahadhari, watumishi wa umma walilazimika kufanya kazi majumbani, kufuatia agizo la Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka, huku wanafunzi wakitakiwa kujisomea majumbani. Shule na vyuo vilifungwa kwa muda, hali iliyosababisha athari kwa kalenda ya masomo na utendaji wa ofisi nyingi za serikali. Mtandao wa intaneti nao ulifungwa, hivyo kufanyia kazi nyumbani nako kulishindikina.
Athari nyingine kubwa ilijitokeza katika sekta ya uchumi. Usafirishaji mizigo uliathirika, hasa katika majiji makubwa kama Dar es Salaam, kutokana na magari ya mizigo kuzuiwa kuingia mjini wakati wa tahadhari. Matokeo yake, soko la chakula lilipata mtikisiko mkubwa.
Leo hii, katika baadhi ya mitaa ya Dar es Salaam, bei za bidhaa za chakula zimepanda kwa kasi ya kutisha: nyanya moja imeuzwa kati ya Sh. 700 na 1,000, fungu la mchicha limefikia Sh. 1,000 hadi 1,500, na baadhi ya viungo kama vitunguu, pilipili hoho na karoti zimepotea kabisa sokoni.
Haya ni matokeo ya mnyororo wa upungufu wa bidhaa unaotokana na usumbufu wa usafiri na hofu ya wafanyabiashara.
Kama Rais Samia asingetangaza kurejesha hali ya kawaida leo, hali ya upungufu wa chakula na ongezeko la bei lingeshuhudiwa zaidi kesho na keshokutwa.
UHARIBIFU WA UCHUMI
Vurugu haziishii tu kwenye uharibifu wa mali. Zinavuruga pia taswira ya taifa mbele ya macho ya dunia. Tanzania imejijengea sifa ya kuwa kisiwa cha amani katika ukanda wa Afrika Mashariki. Inapojitokeza hata chembe ya vurugu, wawekezaji hukosa imani, utalii hupungua na uchumi unatetereka.
Tukumbuke, nchi nyingi za Afrika zimeporomoka kiuchumi kutokana na misukosuko ya kisiasa iliyoanza kwa matukio madogo ya fujo kama haya. Je, tunataka kufika huko?
RAI KWA WANANCHI
Watanzania wote, bila kujali itikadi za kisiasa, tunapaswa kujifunza kutokana na matukio haya. Ni lazima tukubali kwamba tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa sababu ya kuchoma mali, kupora madukani au kuhatarisha maisha ya wengine.
Vurugu haziwezi kubadilisha matokeo ya kisiasa, bali zinaharibu uhusiano wa kijamii na kuvuruga misingi ya taifa lenye umoja. Kama hatutaridhika na jambo fulani, njia za kisheria zipo. Tume ya Uchaguzi, mahakama na vyombo vya usuluhishi vipo kwa ajili ya hayo.
Wanasiasa nao wanapaswa kutoa matamko ya hekima na kujitenga na vitendo vya uchochezi. Viongozi wanaowapenda wananchi wao hawachochei vurugu; wanahubiri utulivu na kuheshimu katiba.
Ni muhimu kwa kila raia kuheshimu taasisi rasmi za nchi kama vyombo vya usalama, tume za uchaguzi (INEC na ZEC) na mahakama. Heshima kwa taasisi hizi ndiyo nguzo ya amani na ustawi wa taifa.
Aidha, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vinapaswa kutumika kama majukwaa ya elimu na ujenzi wa umoja, si zana za kuchochea hofu au kugawa jamii.
Somo kuu la uchaguzi wa 2025 ni kwamba vurugu haina faida. Inaua, inabomoa na inachelewesha maendeleo. Amani, kwa upande mwingine, inaleta fursa, heshima na ustawi wa kweli.
Tanzania imepita katika dhoruba hii kwa jitihada za vyombo vya ulinzi na usalama na utii wa wananchi. Ni wajibu wetu sasa kuhakikisha vurugu za Oktoba 29 hazijirudii tena kamwe.
Tuzingatie maneno ya hekima: “Amani ni tunda la subira na vurugu ni zao la hasira.” Tuchague subira, tuendelee kujenga taifa letu kwa hekima na umoja kwa ajili ya vizazi vya leo na vya kesho.

0 Comments